SHAIRI: NGOJA NGOJA

Standard

IMG-20170730-WA0017.jpg

Ngoja ngoja, yaumiza matumbo

Leta vioja, upigwe kikumbo

Legeza mapaja, uachwe kitambo

Kama huna haja, tupa uone mambo.

 

Chelewa chelewa, mwana si wako

Lala ukilewa, tukutoboe mifuko

Lalama waonewa, usitende, mwiko

Kama hujalewa, hii ngoma si yako.

 

Haraka haraka, haina baraka

Haya alotamka, mvivu hakika!

Kitaka baraka, zitumikie kaka

Kuzifaidi fanaka, kwanza henyeka.

 

Polepole ndio mwendo

Chonde chonde huo so mwendo

Ole ole tatupwa kando

Sie chururu, we ndo ndo ndo!

 

Chembe na chembe huwa mkate

Kitaka utambe taabu ikupate

Kulifaidi sembe shambani upite

Utalipa ng’ombe kabla ya fungate.

 

Uvivu, huleta maumivu

Tamu ya uzembe njaa ikukumbe

Fanya kazi ambaa ubazazi

Omba dua pia chomwa jua.

 

© Paul Mndima

Limetungwa July , 2017

Limetolewa July 31, 2017

Shairi: Njigi na Njege

Standard

Image result for coconut milk

Rafiki na mnafiki, mchungwa na mchenza,

Mitiye na suraze, kutofautisha kwatatiza.

 

Mwizi na mlinzi, karibu wafanana kwa kazi,

Angali wachapa usingizi, wao wafanya kazi.

 

Mbwa na mbwa koko, mnazi na mkoko,

Wafanana sura na mibweko, huyu jasiri yule doko

 

Rijali na choko, shatashata na boko boko

Wote wana viboko, huyu huchapa yule mla mboko

 

Chuki na upendo, hii tisa hii sita

Lau basi si kwa vitendo, apokeae ajua anachopata

 

Jogoo huyu huyu mtetea, majibu ishirini na mosi

Twajuaje ngali yaini kajifungia, subira  subirini msende kasi

 

Msemaji na alojinyamaziya, gazeti na radio

Tofauti njia wanazotumiya, lao moja kusudio

 

Akukwazaye na akupozaye, huyu kipanga huyu mwewe

Asitake bali faidaye, waseme wanajali ila wao sio wewe

 

Pata vyote kosa vtote, hakuna afueni kotekote

Utu, mali si chochote, tamaa hayeshi, ridhika na chochote

 

Niandike yote nighane yote, katu siwezi sema yote

Msoma yote na mwacha yote, katu hawawezi kuelewa vyote.

 

Ukiona njigi utadhani njege, ukinjona njege utadhani njigi

Kifaa kufanana, tui na maziwa.

 

© Paul Mndima

Limeandikwa,  July 3, 2017 na kuhaririwa July 16, 2017.

Limetolewa July 17, 2017.

Picha na livestrong.com

 

 

 

 

SHAIRI: Malenga mwaamba mwafanya nini?

Standard

Image result for POET

Mwayatamka mabadiliko,

Mwayaandika mapambazuko

Mwayaanika ya walo huko

Kwani nyie mwafanya nini?

 

Mwawasema walo juu

Mwawachoma walo wakuu

Twayasoma mno nukuu

Kwani nyie dhambi zenu nini?

 

Kukosoa na kutumbua

Kutoboa na kuumbua

Kuongoa na kutundua

Kwani nyie mwafanywa nini?

 

Mwatuhubiria ya kunena

Mwatughania mnoona

Mwatutambia zenu dhana

Kwani nyie miungu gani?

 

Yenu kalamu na karatasi

Wenu umaamumu maneno basi

Yenu hatamu kusema tu basi

Kwani mikono yenu kutenda kazi?

 

Kuandika kwa mtindo

Kunena pasi vitendo

Mkisikia tu vishindo

Kalamu chini mwachapa mwendo.

 

Malenga msemaji

Malenga mnenaji

Malenga mkosoaji

Malenga malalaji.

 

Asiende atende

Asipende aponde

Sirushe konde chondechonde

Malenga mdosi.

 

Mkosoa vyema ajua bora

Muondoa kiza hashiki bakora

Mwenye hekima hawi mkora

Kwani zaidi ya maneno mna lipi?

 

Limeandikwa na Mwalimu Paul Mndima May 22, 2017

 

Limetolewa 10 July 2017

SAA YA SISI

Standard

Image result for social media

SAA YA SISI

Chonde na saa ya sisi, teke linakujia

Chunga ukikaa na sisi, hasara takufikia

 

Kutwa bofya vya sisi, kazi watufanyia

Kucha kesha na sisi, faida watupatia

 

Jumatatu sisalimie watu, ujumbe tawatumia

Jumanne sivae hata viatu, nje kujitokea.

 

Mkutano siitishe katu, simu tawapigia

Ya nini sumbue watu, baruapepe tawatumia

 

Kitabu kwani cha nini, mtandao maarifa umejaa

Hadithi jioni za nini, kiganjani nasoma nimekaa

 

Barua anaandika nani, pepe bora na haraka charaza

Fotomi namtakia nini instagramu nimezijaza

 

Mkahawani nazungumza nini fesibuku nawapasha

Sokoni naendea nini mtanadaoni tu navishusha.

 

Niacheni na saa ya sisi, teke nalisifia.

 

(C) Paul Mndima.

Saturday, May 6, 2017, ‏‎8:52:21 PM

SIJATUPA MSWAKI WAKO

Standard

SIJATUPA MSWAKI WAKO

tooth brudh

Nakumbuka ulivyoondoka

Hata hukuaga.

Nakumbuka ulivyonichoka

Hata kunimwaga

Nakumbuka ulivyonitenda

Ukaamua kwenda

Nakumbuka ulivyoniponda

Ukanita mdananda

 

Pia

 

Nakumbuka yale mahaba

Nakumbuka zile huba

Nakumbuka mapochopocho

Nakumbuka michokocho.

 

Nakumbuka ufukweni

Nakumbuka ya faraghani

Nakumbuka nyakati zile

Nakumbuka sana yale.

 

Sijasahau matusi yako

Nayakumbuka mashushu yako

Nakumbuka mabusu yako

Nakumbuka maudhi yako.

 

Sijasahau ulivyobamiza mlango

Sijasahau ulivyonikanda mgongo

Nakumbuka ulivyoning’ong’a ming’ong’o

Nakumbuka ulivyonisonya msonyo.

 

Nakumbuka zile asubuhi bafuni

Nakumbuka laini povu mwilini

Nawaza yatarejea hayo tena

Nawaza yatakuwa hayo tena

 

Miaka kenda kumi rudia

Vyote sijajutia

Vyote fanya ukijua

Bado sijautupa mswaki wako.

 

Tuesday, June 6, 2017 5:23:13 PM

Shairi: HISI

Standard

Hisi hisia mie sina hisia.

Njia na nia mie sina hata nia.

Kazi kadhia ndicho nachojua.

 

Ndoa wanaoa mie bado nakodoa.

Wapenzi penzini mie bado ushenzini.

Hatari hatarini midevu kidevuni.

 

Chele nachelewa wote wanaolewa.

Pele wanapelea wazuri wameopolewa.

Ndoa ndoani mie siku yangu lini?

 

Nikimwacha anaolewa na pete anapewa.

Nilomwona ana chawa, jirani kamkuta kanawa.

Haya sasa napagawa adamu mie sina hawa.

 

Hisi hisia sasa nina hisia.

Nina nina nia ila sina njia.

Njia nia hisia sijui wapi naanzia.

 

Jumamosi, Mei 6, 2017

Picha na: http://narrative.ly 

ARUDHI

Standard

 

Kina, nakipenda kina,

Kina kije kikiwa kina mana.

 

Uzani, wala siudhanii,

Uje tu kama waja, siupanii.

 

Muwala, mi nao wala wala,

Kama waja na uje mie sina shida wala.

 

Mshororo sina nao kokoro

Ila sinifunge kwa idadi nitoe kasoro

 

Ubeti usinipe shariti

Eti lazima uwe hivi la sivyo pingiti

 

Arudhi kwangu sio aridhi

Langu tungo najenga kwa kuridhi

 

Lakini, sipotoki sijue napotoka

Nakiweka kina kikija nakipenda

Nauweka mzani ukija navyokwenda

Nakata neno likiwa tamu kulinena

Nafunga ubeti kimaliza nachonena.

 

Sipotoki, kuandika yaso tamu kutamka

Sikurupuki, kughana yaso hamu kunitoka

Sisemi yenye utata, hadhira niikwaze

Sighani yenye ukata, hadhira niipumbaze.

 

Mapingiti, mabutu lau sio masivina

Mavue, manini ila yajieleza kwa kina

 

Sifungwi sijilegezi

Sipingi sipuuzi.

 

Tuesday, May 2, 2017

Picha na: 360connext.com