SHAIRI:KIULIZO

Standard

kiulizo

KIULIZO

Kukicha,

Nikiziangalia mbingu na kuona mwanga,

Napata shauku ya kujua zilivyoumbwa.

Nikitizama jua lavyotoa mwangaza,

Nataka kujua kinacholibebeza.

 

Mchana,

Mawingu yakielea na kusogea,

Jua likitia joto na kukolea,

Mwezi ukififia na kupotea,

Natamani nimwone anowasha na kuzima.

 

Magharibi,

Ndege wanarejea,

Mwanga unafifia,

Mwezi tena watokea,

Jua nalo lafifia.

 

Lela,

Mwezi wanurusha,

Ila hauwezi kupasha,

Nyota zameremeta,

Vimondo vyapitapita.

 

Kiulizo,

Mwanzo, mwisho?

Chanzo, miisho?

Fundi, fundisho?

Mwengi yasemwa,

Lipi hitimisho?

 

© Paul Mndima

Jumatatu, Disemba 18, 2017

 

Advertisements

SHAIRI: MKWEZI

Standard

mkwezi

Mkwezi we kwea

Ila mti una mwisho

Mwenda tezi na omo

Ngama ndio mwisho.

 

Itauma njaa.

Ugali haupikwi mtini

Chini utakuja

Kitako utaketi

Chini ya mti huohuo

Jamvini utajiseti

Mitonge ujijaze .

 

Ukishiba ,

Usingizi utakupata.

Mtini hapalaliki,

Labda uwe popo

Kuanguka ataka nani?

Chini utarudi.

 

Itashika kiu,

Maji yapanda mti?

Wacha sinipe wazimu.

Chini utaja tu

Mferejini  utaenda tu

Lau mtungini

Ila chini utakanyaga tu.

 

 

Utapata haja

Ile mitonge ulosindika.

Muda wake ukifika,

Ile mimaji ulogida,

Mwishowe utachuruza.

Kama nguli,

Chutama ngali juu

Tukuone tupu chini.

 

Sitake kuzaa wewe nani?

Mke umuolee mtini wewe nyani?

Hata umuolee huko juu,

Ya ndoa chumbani.

Faragha sunna,

Kuta zaficha vya ndani.

 

Mtumee!

Nilisahau wewe kiziwi.

Nimekumbuka wewe kipofu.

Unasikia yakuburudishayo.

Unaona yakupendezayo.

Na haya ya kwangu sio.

Wacha nikutazame.

Machweo ije tukuone.

© Paul Mndima

Novemba 2017

SHAIRI: KIONYO

Standard

KIONYO

kionyo

Safiri msafiri kufika yako dhamiri,

Usisahau msafiri safari kitendawili.

Safiri msafiri kufika umetabiri,

Usipumbae msafri kuwasili ni heri.

 

Tabiri mtabiri kesho ngumu kubashiri,

Usisahau mtabiri yote apanga manani.

Tabiri mtabiri ya kesho fikiri,

Kumbuka mtabiri hatujui ataamka nani.

 

Ringa tajiri malizo kwani za nani,

Usisahau tajiri maskini nae binadamu,

Ringa tajiri akiba iko ghalani,

Kumbuka tajiri majanga kaumbiwa mwanadamu.

 

Kula bata kijana tulia ukiwa babu,

Usisahau shababi ujana maji moto.

Lia mbwata kijana si umesoma vitabu,

Usipumbae kijana mtaani kuna moto.

 

Amuru sana Juha mfalme wewe tunakujua,

Usisahau Juha maisha kutesa kwa zamu.

Kufuru sana Juha waache makapuku kwenye jua,

Sisahau Juha ukishuka utarudi humu.

 

Ghani sana mshairi kalamu yako mshairi,

Usisahau ushairi fasihi ya usawiri.

Ghali kusitiri ukafiri,

Gharamaye kubwa mshairi.

 

©Paul Mndima

APC 30th Jan ‘17

 

 

 

 

SHAIRI:AFYA NJEMA NI TUNU

Standard

AFYA NJEMA NI TUNU

afya njema

Nahesabu misumari, iliyoezeka paa hili

Najigeuza kwa tahadhari, nikimlilia Jalali

Afya njema ni johari, ni vyema kujijali

Maradhi yasikie kwa jirani, ukukose mkuki huu.

 

Naziangalia tembe, na bilauri hii la maji

Nimenyong’onyea mzembe, umekwisha ujuaji,

Kabla sijameza niombe, ziniponye nahitaji

Maradhi yasikie kwa jirani, ukukose mkuki huu.

 

Naitizama sahani, hamu na chakula sina

Asisitiza chochote tumboni, tabibu ila kazi kutafuna

Kuku, samaki na biriani, ulafi wote hakuna

Maradhi yasikie kwa jirani, ukukose mkuki huu.

 

***

 

Maradhi maruwani, yakipanda tawekwa baalani

Maradhi tafurani, yatowesha amani kama tufani

Maradhi subiani, yachafua roho za wenye imani

Maradhi jahanamu, ngali hai nachomwa mwanadamu.

 

Jipende ndugu jipende, jilishe halua na tende,

Matunda muhimu yapende, kabla hujalala kitanda

Mboga nazo patana nazo, kupungua damu sio mchezo

Maji ya nanasi sharubati, lahaula jitendee haki jipeti.

 

Wanga nazao pia manga, upate nguvu za kupuyanga

Protini usizitupe mitini, nyama mharagwe kwenye sahani

Mtindi, maziwa, jibini, mafuta yatia joto mwilini

Vitamini chumvi na majani, yafaa sana pia madini

 

Usile vichafu pia, donoa donoa hatma jutia,

Usinywe vileo pia, vyashusha afya nakwambia

Usichome chome pia, vingine utajanasia

Usifunue funue pia, vichafu visijeingia

 

Jioni pia kimbia, sikae sana tembea

Kutwaa tu kujilalia, viungo taja lemea

Puyanga pia tokwa na jasho

Kitambi unene miyeyusho.

 

Afya njema ni johari, ni vyema kujijali

Tuishi kwa tahadhari, tuombe nema za Jalali.

© Paul Mndima

Septemba 22, 2017

SHAIRI: Mama Sele na Mama Hamisi

Standard

Mama Sele na Mama Hamisi

 

Yalaaaa!

Mama Sele na Mama Hamisi wanasutana.

Majirani hatulali, kukuru kakara wanatukana.

Mtumee!

 

Ingefaa ningehama mtaa, laa ya urithi nyumba nayokaa.

Sasa karibuni sita saa, tititi usiku kiza totoro,

Hapana hata dalili, wajadi hawa kuesha mgogoro.

Kisa si kisa, visa visa tu kuzua mikasa,

Wake wa mume mmoja mabibi wa Mzee Kipara,

Washona dela moja wagombea majora,

Wasuka mkeka mmoja  kuti wagombea kulipara,

Domo walisha moja, ya nini kugombea mitonge?

Wacha mie nijikune kipara,

Tu nitizame ugomvi wa mafara.

© Paul Mndima

Limeandikwa , Mei 2, 2017  

Limetolewa Septemba 25 2017

SHAIRI:DUNIA KICHAA

Standard

dunia kichaa 3

Kwenye hii dunia kichaa

Tunaishi na watu, tunaishi na wanyama.

Sio wa porini tu, hata wale yunaowaita baba na mama.

Tofauti, sio maumbile yao, tabia zao na mienendo yao,

Kwa jinsi ya kuumbwa twafanana nao,

Ila utu ndio tofauti kati ya sisi na wao.

 

Kwenye hii dunia kichaa,

Wapo miungu,

Nikisema miungu sina maana

Ya wale tunao waabudu,

Hasha

Bali wale wanaoamua juu ya maisha ya wengine.

Wakisema washa, inawaka, zima inazimwa

Hao wanaamua nani afike kesho nani aishie leo

 

Kwenye hii dunia kichaa

Tunapigana, tunabishana tunauana

Kisa?

Miungu, dini na manabii tusiowajua,

Tunasikia hadithi tu na bwajaja za majukwaa.

 

Kwenye hii dunia kichaa

Kaka anavaa kama dada

Dada anavaa kama kaka

Kaka kawa kaka poa

Dada kawa dada poa

Ukikuta wamejipodoa

Hujui nani ni nani

Yoyote unaeza opoa.

 

Kwenye hii dunia kichaa,

Giningi si giningi

Mambo ngijinginji hakuna misingi

Shaghalabaghala,

Akisema hatupingi

Bi. Kirembwe kavua shungi

Kavalia suti

Fimbo yake shilingi

Masikhara hana

Kukutoboa havungi

Wasemavyo wenyewe,

Yu avuta mibangi

 

Kwenye hii dunia kichaa,

Zipo sehemu

Za watu fulani

Na za watu fulani fulani.

Ambapo, watu fulani hawastahili kufika kwa watu fulani fulani

Lakini akina fulani fulani

Wanaweza kuwabwakura akina fulani

Mahali fulani palipo pao!

Ujahili mtupu.

 

Kwenye hii dunia kichaa,

Tunapimwa uzito.

Lakini kuna mizani za akina fulani fulani

Na akina fulani nao wana yao mizani

Huku uzani unasema ratili ni vibaba fulani

Huku vibaba fulani

Hivyo wapo wenye vitambi

Na tupo matambitambi.

 

Kwenye hii dunia kichaa,

Kuna maisha,

Lakini si ya wote kuishi,

Wapo wanaoishi

Tupo tunokula matapishi

Ya wale wanaoishi

Na sie hatuna hata ubishi

Wale wakisema sisi hatubishi.

Yafaa nini basi kuishi

Kwenye hii dunia kichaa.

 

©Paul Mndima

Limetungwa: ‎Julai 18, ‎2017