SHAIRI:AFYA NJEMA NI TUNU

Standard

AFYA NJEMA NI TUNU

afya njema

Nahesabu misumari, iliyoezeka paa hili

Najigeuza kwa tahadhari, nikimlilia Jalali

Afya njema ni johari, ni vyema kujijali

Maradhi yasikie kwa jirani, ukukose mkuki huu.

 

Naziangalia tembe, na bilauri hii la maji

Nimenyong’onyea mzembe, umekwisha ujuaji,

Kabla sijameza niombe, ziniponye nahitaji

Maradhi yasikie kwa jirani, ukukose mkuki huu.

 

Naitizama sahani, hamu na chakula sina

Asisitiza chochote tumboni, tabibu ila kazi kutafuna

Kuku, samaki na biriani, ulafi wote hakuna

Maradhi yasikie kwa jirani, ukukose mkuki huu.

 

***

 

Maradhi maruwani, yakipanda tawekwa baalani

Maradhi tafurani, yatowesha amani kama tufani

Maradhi subiani, yachafua roho za wenye imani

Maradhi jahanamu, ngali hai nachomwa mwanadamu.

 

Jipende ndugu jipende, jilishe halua na tende,

Matunda muhimu yapende, kabla hujalala kitanda

Mboga nazo patana nazo, kupungua damu sio mchezo

Maji ya nanasi sharubati, lahaula jitendee haki jipeti.

 

Wanga nazao pia manga, upate nguvu za kupuyanga

Protini usizitupe mitini, nyama mharagwe kwenye sahani

Mtindi, maziwa, jibini, mafuta yatia joto mwilini

Vitamini chumvi na majani, yafaa sana pia madini

 

Usile vichafu pia, donoa donoa hatma jutia,

Usinywe vileo pia, vyashusha afya nakwambia

Usichome chome pia, vingine utajanasia

Usifunue funue pia, vichafu visijeingia

 

Jioni pia kimbia, sikae sana tembea

Kutwaa tu kujilalia, viungo taja lemea

Puyanga pia tokwa na jasho

Kitambi unene miyeyusho.

 

Afya njema ni johari, ni vyema kujijali

Tuishi kwa tahadhari, tuombe nema za Jalali.

© Paul Mndima

Septemba 22, 2017

Advertisements

SHAIRI: Mama Sele na Mama Hamisi

Standard

Mama Sele na Mama Hamisi

 

Yalaaaa!

Mama Sele na Mama Hamisi wanasutana.

Majirani hatulali, kukuru kakara wanatukana.

Mtumee!

 

Ingefaa ningehama mtaa, laa ya urithi nyumba nayokaa.

Sasa karibuni sita saa, tititi usiku kiza totoro,

Hapana hata dalili, wajadi hawa kuesha mgogoro.

Kisa si kisa, visa visa tu kuzua mikasa,

Wake wa mume mmoja mabibi wa Mzee Kipara,

Washona dela moja wagombea majora,

Wasuka mkeka mmoja  kuti wagombea kulipara,

Domo walisha moja, ya nini kugombea mitonge?

Wacha mie nijikune kipara,

Tu nitizame ugomvi wa mafara.

© Paul Mndima

Limeandikwa , Mei 2, 2017  

Limetolewa Septemba 25 2017

SHAIRI:DUNIA KICHAA

Standard

dunia kichaa 3

Kwenye hii dunia kichaa

Tunaishi na watu, tunaishi na wanyama.

Sio wa porini tu, hata wale yunaowaita baba na mama.

Tofauti, sio maumbile yao, tabia zao na mienendo yao,

Kwa jinsi ya kuumbwa twafanana nao,

Ila utu ndio tofauti kati ya sisi na wao.

 

Kwenye hii dunia kichaa,

Wapo miungu,

Nikisema miungu sina maana

Ya wale tunao waabudu,

Hasha

Bali wale wanaoamua juu ya maisha ya wengine.

Wakisema washa, inawaka, zima inazimwa

Hao wanaamua nani afike kesho nani aishie leo

 

Kwenye hii dunia kichaa

Tunapigana, tunabishana tunauana

Kisa?

Miungu, dini na manabii tusiowajua,

Tunasikia hadithi tu na bwajaja za majukwaa.

 

Kwenye hii dunia kichaa

Kaka anavaa kama dada

Dada anavaa kama kaka

Kaka kawa kaka poa

Dada kawa dada poa

Ukikuta wamejipodoa

Hujui nani ni nani

Yoyote unaeza opoa.

 

Kwenye hii dunia kichaa,

Giningi si giningi

Mambo ngijinginji hakuna misingi

Shaghalabaghala,

Akisema hatupingi

Bi. Kirembwe kavua shungi

Kavalia suti

Fimbo yake shilingi

Masikhara hana

Kukutoboa havungi

Wasemavyo wenyewe,

Yu avuta mibangi

 

Kwenye hii dunia kichaa,

Zipo sehemu

Za watu fulani

Na za watu fulani fulani.

Ambapo, watu fulani hawastahili kufika kwa watu fulani fulani

Lakini akina fulani fulani

Wanaweza kuwabwakura akina fulani

Mahali fulani palipo pao!

Ujahili mtupu.

 

Kwenye hii dunia kichaa,

Tunapimwa uzito.

Lakini kuna mizani za akina fulani fulani

Na akina fulani nao wana yao mizani

Huku uzani unasema ratili ni vibaba fulani

Huku vibaba fulani

Hivyo wapo wenye vitambi

Na tupo matambitambi.

 

Kwenye hii dunia kichaa,

Kuna maisha,

Lakini si ya wote kuishi,

Wapo wanaoishi

Tupo tunokula matapishi

Ya wale wanaoishi

Na sie hatuna hata ubishi

Wale wakisema sisi hatubishi.

Yafaa nini basi kuishi

Kwenye hii dunia kichaa.

 

©Paul Mndima

Limetungwa: ‎Julai 18, ‎2017

 

 

SHAIRI: FUMBO

Standard

fumbo

Fumbo fumbo,

Fumbua!

Fumbo mfumbie mjinga,

Mwerevu nitakuumbua.

 

Fuga mbwa, mpake rangi ya sungura,

Mfunge na mnyororo wa dhahabu,

Hutufichi babu.

Atataka nyama tu.

Atabweka tu babu.

 

Fumbo fumbo,

Fumbua!

 

Fuga nyani,

Mpake na wanja, na mpodoe podoe,

Mvishe na gauni la zambarau,

Wamdanganya nani babu?

Atataka ndizi tu.

Babuuu! Atapandia miti tu babu

 

Fumbo fumbo,

Fumbua!

 

Jenga nyumba,

Paka na rangi za kifalme,

Weka na samani za thamani,

Wacha kujipa ujinga babu,

Nyumbani watu babu.

Itakuwa nyumba tu,

Huwezi kupaita nyumbani katu.

 

Fumbo fumbo,

Fumbua!

 

Soma babu,

Soma sana babu.

Weka na madigirii na maporofesa babu,

Pita hutuamkii jidai ringa babu,

Ila kama haikusaidii,

Elimu ya nini babu?

Elimu ukombozi babu.

 

Fumbo fumbo,

Fumbua!

 

Mwambie utamuoa babu,

Tangaza na ndoa babu,

Hakikisha unachojoa babu,

Mpeleke maskani babu,

Hakikisha unatoboa babu,

Ukishakojoa babu, mahari ya nini kutoa babu?

Nenda tu kawinde kwengine babu.

 

Fumbo bwana eeh!

Fumbo mfumbie mjinga babu,

Mwerevu nitakuumbua babu.

 

Fumbo fumbo,

Fumbua!

 

Mwaga hela mwaga sera babu,

Zimiminie zimiminike tupatie zitushike babu,

Machozi tumiminie,

Tizi tupigie babu,

Ahadi tutambishie babu,

Hila zako tulainishie babu.

Ukishafika juu babu, huku we tunyee tu babu,

Kwani sie watu babu?

 

Fumbo mfumbie mjinga babu

Mwerevu ntakuumbua babu.

Eeeh bwana wee!

 

Fumbo fumbo,

Fumbua!

 

Piga kazi babu,

Sota sana babu,

Kaza buti babu,

Pigika henyeka babu,

Ikifika jioni babu, pigisha raundi babu,

Rudi nyumba ni mweupeeee,

Amina kakukuna kakupuna zote kachuna,

Kesho rudia tena babu.

 

Fumbo fumbo,

Fumbua!

 

Podoka mama podoka,

Weka wanja na midomo rangi paka,

Kikundi kina mama leo muhimu fika,

Kata kona kwa Rama mpemba,

Urudi nywele tim tim,

Na rangi zimefutika,

Jumamosi tena babu wee!

Fala kala kalala kalalama

Vya fala kala mzee Rama.

 

Hahahahaaa!

 

Fumbo fumbo,

Fumbua!

Fumbo mfumbie mjinga babu,

Mwerevu nitakuumbua babu.

 

©Paul Mndima

Limetungwa Agosti 26, 2017

SHAIRI: NGOJA NGOJA

Standard

IMG-20170730-WA0017.jpg

Ngoja ngoja, yaumiza matumbo

Leta vioja, upigwe kikumbo

Legeza mapaja, uachwe kitambo

Kama huna haja, tupa uone mambo.

 

Chelewa chelewa, mwana si wako

Lala ukilewa, tukutoboe mifuko

Lalama waonewa, usitende, mwiko

Kama hujalewa, hii ngoma si yako.

 

Haraka haraka, haina baraka

Haya alotamka, mvivu hakika!

Kitaka baraka, zitumikie kaka

Kuzifaidi fanaka, kwanza henyeka.

 

Polepole ndio mwendo

Chonde chonde huo so mwendo

Ole ole tatupwa kando

Sie chururu, we ndo ndo ndo!

 

Chembe na chembe huwa mkate

Kitaka utambe taabu ikupate

Kulifaidi sembe shambani upite

Utalipa ng’ombe kabla ya fungate.

 

Uvivu, huleta maumivu

Tamu ya uzembe njaa ikukumbe

Fanya kazi ambaa ubazazi

Omba dua pia chomwa jua.

 

© Paul Mndima

Limetungwa July , 2017

Limetolewa July 31, 2017