ZA MWIZI

Standard

Za Mwizi

Maskini kipata tako hulia mbwata,

Wali shata shata  kwa mafuta ya mbata,

Keti kitako nabwata nikuhadithie kilichonipata.

 

Ilikuwa kama sita, miaka ilopita,

Baada ya masika, mvua zilikatika,

Nikatoka nikenda, kwa yule bibie niliempenda,

Hapo mazao nishauza, mihela kiroba naburuza.

 

Bibie mwenyewe mkewe mpemba, yule mwuza mitumba,

Alokuwa akiimba, sokoni kujigamba,

Mkewe nilimlamba, nikamuona mshamba,

Sikujua ananichimba, ukweli kuukumba.

 

Mke wangu nilimuaga, naenda mkwajuni kujua kunani,

Yule mpemba sokoni, mimi na mkewe vinjari nyumbani

Mie mpaka kwake hodi, karibu ndani kwa uturi na udi,

Nikala utamu kunoga, asali faudu bila woga.

 

Thatlathini na kenda ikafika, arubaini kuwadia,

Hamadi jembe naweka, shimoni mpini kunasia,

Sivute uje katika, mtumee mpemba kaingia,

Mke wangu kiuno kashika, na jumbe wote kushuhudia.

 

Aibu menifika, mpemba kanishika,

Mkewe machozi yamtoka, mumewe kakasirika,

Mke wangu alishacharuka, ananidai talaka,

Mtaani wote wanicheka, fedheha nimejitwika.

 

Ama kweli haramu, yatia doa kuliko damu,

Hata hizi pesa za kiburi, sinazo tena jeuri,

Aheri aibu kuliko fedheha, kweli fedha fedheha,

Kila mmoja kunizomea, kati yao kondoo mimi bweha.

 

Haya sasa wacha anasa, jifunze kwa wangu makasa,

Kama unabisha endelea kupata, paka siku utaponasa,

Ndo ujifunze njia inayopasa, ukishapatwa na mkasa,

Au upate maradhi ya kisasa, ukishalamba garasa.

 

Paul Mndima

Thursday, November 10, 2016. 10:20:07 PM

PicCred: images5.aplus.com

 

 

 

 

 

 

 

 

 

NYEUPE/NYEUSI

Standard

NYEUPE NYEUSI

 

Hali si hali mpaka iwe shwari ama shari

Kwenye kitu kuna mawili, kipo au hakipo

Je, ilinyesha haikunyesha, zaidi ya hapo hakuna la kuonesha.

Kuna mawili, moja au sifuri, ubaya au uzuri

Nyeusi nyeupe, ku giza au ku mwanga kweupe.

 

Lakini, yu aamua nani haya yote?

Na yu aamua kwa nani haya yote?

Kwani nini tatizo tukiuita wema kuwa ubaya?

Kwani kipi kigezo cha wema na ubaya?

 

Wataka kusema yalijizukia tu mambo haya?

Au wataka sema tuliyapokea tu mambo haya?

Hamkuuliza?

Au mlipokea tu mkala cha moto pasi kupuliza?

Yenu kutimiza,

Hakusumbua bongo, kama watoto mkaigiza.

 

Iko sababu, chunguza

Usione ajabu, ukikuta unaburuzwa.

 

Uliza yote, usikubali yote.

Pokea yote, usishikilie yote.

 

Hakuna giza, aidha uko mwanga au la

Haiko baridi, aidha liko joto au la

Basi hata ubaya hakuna, ni wema tu unatoweka

Au basi hakuna wema, ni ubaya tu unatoweka

kipi ni kipi?

 

Hebu subiri, mbona nami nachanganyikiwa?

Haya nahubiri, mbona nami yanisumbuwa?

 

Ebo! Najichoshea nini kwani?

Watu wenyewe ndio nyie msohoji imani?

 

Wacha nende zangu!

Bora puuzia tu maneno yangu.

 

Wakiuliza nani kasema haya, wala usinitaje.

© Paul Mndima Aprili 24, 2017

 

Photo Credits: img.clipartfest.com 

JOGOO WA MAYAI

Standard

Jogoo wa mayai

JOGOO

Napenda mayai, nikila nafurahi,
Kwa afya natumai, chajio staftahi,
Ndio mana sokoni, leo mie mwendaji,
Nijiwekee bandani, afae kwa mahitaji.

Nichagulie mkubwa, atage makubwa,
Watoto kwa wakubwa, asubuhi haufai ubwabwa,
Wafaidi kwa utamu, afya tele kwa familiya
Sikaidi umuhimu, lishe bora najitakiya

Muuzaji kanipatiya, mkubwa kaniambiya,
Anafaa kunitagiya, mayai kujiliya,
Lakini ni jogoo, kabebesha na udundu,
Naambiwa nijipe moyo, kutaga atamudu.

Nimlishe kwa wingi, pumba na mashudu,
Mayai ni mengi, utamu nitaufaudu,
Mchicha na mahindi, vitamini na madini
Kufuga niwe fundi, si kazi ya utani.

Nikanunua vyakula, madawa na chanjo,
Nikawa mkao wa kula, kuyapokea nikawa chonjo,
Kwa hamu na shauku, mafanikio kuyaonja,
Huku nikimlea kuku, nijisifu mjanja.

Nikapata na mayowe, kila ifikapo asubuhi,
Mapema wika jimbi, shuka tupa chini alinisihi,
Sikuhitaji hata saa, akiwika tu yatosha
Hata wa swala wasaa, habari alinipasha.

Haya sasa yapata, siku hamsini na kadhaa,
Hata moja sijapata, zaidi ya kelele na kadhia,
Mabawa asubuhi akipepeta, mavi uwani kuninyea
Na chakula chema anapata, me bado najikondea.

Walisema, ng’ombe wa maskini hazai,
Na mimi naongeza, jogoo kutaga haifai,
Hata umlishe sima, kamwe hatagi yai
Usisikize wanayosema, wauzaji ni walaghai.

Bora kumchinja, supu ninywe badala ya chai,
Nibaki na safi kiwanja, bora hata kununua mayai
Hasara tena sitaki, kikuu nakitupa kinyemi nakiendea
Yapata siku nne baki , gulioni tena kuelekea.

Wakati huu, sitakosea.

Wakikuuliza nani kasema haya, waambie ni mwalimu Paul Mndima
Novemba 2016 – Aprili 2017

Picture credit: thehookiepookie

PANZI NA KUNGURU

Standard

PANZI NA KUNGURU

art.jpg

Panzi, alikuwapo panzi. Na jamii yake.
Kunguru, alikuwapo kunguru. Na jamii yake.

Panzi na jamii yake walijua kujificha,
Kunguru na jamii yake njaa kutwa kucha.

Kunguru na jamii yake walinoa makucha,
Panzi na jamii yake kuwafanya mabucha.

Basi jamii yake, ikamtuma kunguru,
Kwenda kwa Panzi na jamii yake kuomba udhuru,

Kunguru, na jamii yake wakaomba uchumba,
Panzi, na jamii yake wakampokea mchumba.

Kunguru, na jamii yake wakaandaa karamu,
Panzi na jamii yake wakahudhuria kwa hamu

Panzi na jamii yake wakashiba hakika,
Kunguru, na jamii yake wakafurahi hakika

Mwisho ukafika, sherehe kuhitimika,
Kunguru kamshika, panzi kampika.

Jamii ya kunguru nayo kufaidika.
Jamii ya panzi yote kuifyeka.

Funzo, adui ajaye kwa upanga, ni bora kuliko ajaye mikono nyuma.

Wakikuuliza ni nani kasema haya, waambie ni mwalimu Paul Mndima

Wednesday, April 5, 2017 7:22:30 AM

MTEMA KUNI

Standard

 

Image result for african man cutting trees

MTEMA KUNI

Mtema kasema, hodari yeye tangu mapema,

Panga mkononi lazima, ni hatari usijaribu mpima,

Makaliye pangale, hayasemeki asilani,

Atakaye akale, kuni kwake asikose habadani.

 

Mtema kafyeka misitu, kafyerenga hadi chatu,

Haishi midomoni mwa watu, nyikani bila viatu,

Kachoronga hadi magogo, mtema hana wema na miti,

Kavuruga hadi mipingo, mtema ashindwe na vijiti?

 

Mtema mungu mtu, miti imwone imwabudu,

Mtema ana nguvu huyu mtu, vichaka vyamsujudu,

Mtema mfalme wa kukata, hata mivule haimpi shaka,

Mtema bila hata ngata, tita kujitwika hana mashaka.

 

Mtema kajisahau, kajawa na dharau,

Mtema angalau, avae kiatu cha sendeu,

Chaka kalivamia, mjanja yeye nakwambia,

Panga lake keshajinolea, kwa madaha kashambulia.

 

Thalathini na kenda jana, arubaini leo kufikia,

Kwa juhudi huyu kijana, mabinti kuwaoneshea,

Wakipita kumsalimu, madaha azidisha kutema,

Si kushangaa aone utamu, lahaula mkono kautema.

 

Mtema sasa si mtema tena, mtema sasa mtema tema,

Majuto jutia afanyeje tena, mjukuu kilema cha mapema,

Ama kweli ukilewa sifa, fedheha yakungojea kukulima,

Mtema hata leo akifa, tutamkumbuka kama kilema.

 

Wakiuliza nani kaandika haya, waambie ni Mwl. Paul Mndima

paulmndima@yahoo.com

+255658152022

© Februari 2017

Photo: http://twistedsifter.com/tag/africa/page/3/

 

VIDEO: NAFSI YANGU

Standard

Shairi hili nililisoma siku ya ijumaa 31 Machi 2017 kwenye usiku wa ushairi ulioandaliwa na Poetry 255 na kufanyika Soma Book Cafe.
Nikiwa kama mwanachama wa Arusha Poetry Club (APC) nilipata mwaliko wa kuwashirikisha wahudhuriaji nilichoandaa.
Hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kusoma shairi mbele za watu kwa hivyo mnisamehe kwa kutoweza kufanya kwa utaalam, bado najifunza.
Karibuni kusikiliza na shirikisha wengine pia.
Asante.

SHAIRI: MIMI NDIO BABA, MWINGINE AWE NANI?

Standard

Mimi ndio baba mwengine awe nani?

father-and-son-003.jpg

Shairi nawaandikia, enyi watu wa duniani,

Baba muhimu kwa familia, sio mama tu mumthamini,

Mimi ndio baba, mwengine awe nani?

 

Mimi ndio baba, kichwa nyumbani,

Uongozi kwangu haiba, naongoza walo ndani,

Mimi ndio baba, mwengine awe nani.

 

Msaidizi wangu mama, alowaleta duniani,

Uchungu ulimuuma, niliwaweka mimi changoni,

Mimi ndio baba, mwengine awe nani?

 

Njaa ikiwashika, macho yao kwangu,

Kuwalisha kuwavika, yote majukumu yangu,

Mimi ndio baba, mwengine awe nani?

 

Hakuna kama mama, kweli hata mimi nasema,

Lakini hata huyo mama, atoka kwa babaye lazima,

Mimi ndio baba, mwengine awe nani?

 

Uchungu wa mwana, methali ya waswahili,

Aujuae mlea mwana, wote haki wastahili,

Mimi ndio baba, mwengine awe nani?

 

Nailinda familia, nawakumbata wakilia,

Hata janga likifikia, wote huniangalia,

Mimi ndio baba, mwengine awe nani?

 

Mungu kanipatia, madaraka wote kuzidia,

Hata mfalme na malikia, baba yao wanamuamkia,

Mimi ndio baba, mwngine awe nani?

 

Tamati tamatiya, shairi namalizia,

Mama muhimu nakwambiya, bila baba hajatimia.

Mimi ndio baba, mwengine awe nani?

 

Paul Mndima 2016