TUNGO ZAO ZA OVYO.

Standard
Shairi hili ni utungo wake Dotto Rangimoto Chamchua, alitushirikisha utungo huu katika kundi nami nikaupenda, nikaona ni jambo jema kama nikikushirikisheni nanyi mpate kile asemacho.
Shairi hili laturudisha wakati ule wa enzi za mgogoro wa ushairi, kipindi ambacho palikuwa na mvutano kati ya watunzi wa kimapokeo na wale wa kimamboleo.
Nadhani ni shairi amabalo laweza kuamsha hisia, hasa za wale walengwa wa shairi hili na kuleta mjadiliano, ambalo si jambo baya. Una maoni gani juu ya hili? Hebu soma halafu utupatie ujumbe wako.
Karibu.
|
|
TUNGO ZAO ZA OVYO.
 |
Mwanga mvamia pungo, kilingeni kwa mganga,
Sawa na watunga tungo, huku wakiziboronga,
Kisha kwa zao borongo, wajivike umalenga,
Bora lende si kutunga, ni kuzidhulumu tungo.
Padri mchora kisango, na hirizi kuzifunga,
Sawa na wabeba bango, la kujinadi watunga,
Kumbe watungazo nongo, hawajijuwi mabunga,
Bora lende si kutunga, ni kuzidhulumu tungo.
 |
Shetani hasa kibwengo, saum anapofunga,
Sawa na wao utungo, wa kubananga bananga,
Kisha wajipa kiwango, kama kile cha wahenga,
Bora lende si kutunga, ni kuzidhulumu tungo.
 |
Mpishi asiye bongo, mpika wali na chunga,
Sawa na wao mpango, wa tungo wanazotunga,
Tungo mapengo mapengo, kisha waziita kunga,
Bora lende si kutunga, ni kuzidhulumu tungo.
|
Latakikana komango, na chungio la kuchunga,
Waipinde na migongo, ndipo watapata unga,
Wakileta rongorongo, hawapati japo chenga,
Bora lende si kutunga, ni kuzidhulumu tungo.
 |
Kibeku pamwe na ungo, wangakazana kuwanga,
Halitimu lao lengo, la kulitawala anga,
Watavundika migongo, anga mwenyewe kipanga,
Bora lende si kutunga, ni kuzidhulumu tungo.
|
Kwenda vitani na gongo, ama kuenda na panga,
Sawa kutaka ulingo, na mimi Jini Kinyonga,
Kama wanao ubongo, wazitunge za kulenga,
Bora lende si kutunga, ni kuzidhulumu tungo.
 |
Mwisho hiki ni kigongo, kimekuja kuwagonga,
Wao wenye tongotongo, wasiojuwa kutunga,
Ngoma hii kisamango, kiroja wacheza vanga,
Bora lende si kutunga, ni kuzidhulumu tungo.
 |
09 Meyi 2017 Jumanne 15:14
#JiniKinyonga
NjanoTano
Dotto Rangimoto Chamchua
Whatsapp 0622845394 Morogoro.
|
Natumai umepata kitu hapo, kusoma Zaidi mashairi ya ndugu Rangimoto, tembelea ukurasa wake wa Facebook Mashairi ya Rangimoto
Asanteni.
Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s