SHAIRI:KIULIZO

Standard

kiulizo

KIULIZO

Kukicha,

Nikiziangalia mbingu na kuona mwanga,

Napata shauku ya kujua zilivyoumbwa.

Nikitizama jua lavyotoa mwangaza,

Nataka kujua kinacholibebeza.

 

Mchana,

Mawingu yakielea na kusogea,

Jua likitia joto na kukolea,

Mwezi ukififia na kupotea,

Natamani nimwone anowasha na kuzima.

 

Magharibi,

Ndege wanarejea,

Mwanga unafifia,

Mwezi tena watokea,

Jua nalo lafifia.

 

Lela,

Mwezi wanurusha,

Ila hauwezi kupasha,

Nyota zameremeta,

Vimondo vyapitapita.

 

Kiulizo,

Mwanzo, mwisho?

Chanzo, miisho?

Fundi, fundisho?

Mwengi yasemwa,

Lipi hitimisho?

 

© Paul Mndima

Jumatatu, Disemba 18, 2017

 

Advertisements

SHAIRI: MAISHA

Standard

maisha-designstyle-i-love-m

Maisha,

Keki safi ya shubiri,

Ilopambwa na utando mwembamba wa sukari

Rangi nzuri za waridi

Na arufu tamu ya asumini.

 

Maisha tunaishi watu,

Maisha ni ya watu,

Maisha yana tabu,

Tabu ni za watu

Na watu ndio sisi.

 

Usilie utulie,

Usiwaze jiliwaze

Usijute yakukute

Usichoke sifadhaike

Jipe moyo yashinde hayo.

 

Hakuna aso na shida

Hakuna yasomkwida

Hakuna ano faida

Hata moja siku asipate shida.

 

Jikaze, jifunze

Jitume, jitunze

Jijuze, usipuuze

Na mwisho, yote yatakuwa sawa.

© Paul Mndima – 2017

SHAIRI: MKWEZI

Standard

mkwezi

Mkwezi we kwea

Ila mti una mwisho

Mwenda tezi na omo

Ngama ndio mwisho.

 

Itauma njaa.

Ugali haupikwi mtini

Chini utakuja

Kitako utaketi

Chini ya mti huohuo

Jamvini utajiseti

Mitonge ujijaze .

 

Ukishiba ,

Usingizi utakupata.

Mtini hapalaliki,

Labda uwe popo

Kuanguka ataka nani?

Chini utarudi.

 

Itashika kiu,

Maji yapanda mti?

Wacha sinipe wazimu.

Chini utaja tu

Mferejini  utaenda tu

Lau mtungini

Ila chini utakanyaga tu.

 

 

Utapata haja

Ile mitonge ulosindika.

Muda wake ukifika,

Ile mimaji ulogida,

Mwishowe utachuruza.

Kama nguli,

Chutama ngali juu

Tukuone tupu chini.

 

Sitake kuzaa wewe nani?

Mke umuolee mtini wewe nyani?

Hata umuolee huko juu,

Ya ndoa chumbani.

Faragha sunna,

Kuta zaficha vya ndani.

 

Mtumee!

Nilisahau wewe kiziwi.

Nimekumbuka wewe kipofu.

Unasikia yakuburudishayo.

Unaona yakupendezayo.

Na haya ya kwangu sio.

Wacha nikutazame.

Machweo ije tukuone.

© Paul Mndima

Novemba 2017

SHAIRI: KIONYO

Standard

KIONYO

kionyo

Safiri msafiri kufika yako dhamiri,

Usisahau msafiri safari kitendawili.

Safiri msafiri kufika umetabiri,

Usipumbae msafri kuwasili ni heri.

 

Tabiri mtabiri kesho ngumu kubashiri,

Usisahau mtabiri yote apanga manani.

Tabiri mtabiri ya kesho fikiri,

Kumbuka mtabiri hatujui ataamka nani.

 

Ringa tajiri malizo kwani za nani,

Usisahau tajiri maskini nae binadamu,

Ringa tajiri akiba iko ghalani,

Kumbuka tajiri majanga kaumbiwa mwanadamu.

 

Kula bata kijana tulia ukiwa babu,

Usisahau shababi ujana maji moto.

Lia mbwata kijana si umesoma vitabu,

Usipumbae kijana mtaani kuna moto.

 

Amuru sana Juha mfalme wewe tunakujua,

Usisahau Juha maisha kutesa kwa zamu.

Kufuru sana Juha waache makapuku kwenye jua,

Sisahau Juha ukishuka utarudi humu.

 

Ghani sana mshairi kalamu yako mshairi,

Usisahau ushairi fasihi ya usawiri.

Ghali kusitiri ukafiri,

Gharamaye kubwa mshairi.

 

©Paul Mndima

APC 30th Jan ‘17

 

 

 

 

SHAIRI:AFYA NJEMA NI TUNU

Standard

AFYA NJEMA NI TUNU

afya njema

Nahesabu misumari, iliyoezeka paa hili

Najigeuza kwa tahadhari, nikimlilia Jalali

Afya njema ni johari, ni vyema kujijali

Maradhi yasikie kwa jirani, ukukose mkuki huu.

 

Naziangalia tembe, na bilauri hii la maji

Nimenyong’onyea mzembe, umekwisha ujuaji,

Kabla sijameza niombe, ziniponye nahitaji

Maradhi yasikie kwa jirani, ukukose mkuki huu.

 

Naitizama sahani, hamu na chakula sina

Asisitiza chochote tumboni, tabibu ila kazi kutafuna

Kuku, samaki na biriani, ulafi wote hakuna

Maradhi yasikie kwa jirani, ukukose mkuki huu.

 

***

 

Maradhi maruwani, yakipanda tawekwa baalani

Maradhi tafurani, yatowesha amani kama tufani

Maradhi subiani, yachafua roho za wenye imani

Maradhi jahanamu, ngali hai nachomwa mwanadamu.

 

Jipende ndugu jipende, jilishe halua na tende,

Matunda muhimu yapende, kabla hujalala kitanda

Mboga nazo patana nazo, kupungua damu sio mchezo

Maji ya nanasi sharubati, lahaula jitendee haki jipeti.

 

Wanga nazao pia manga, upate nguvu za kupuyanga

Protini usizitupe mitini, nyama mharagwe kwenye sahani

Mtindi, maziwa, jibini, mafuta yatia joto mwilini

Vitamini chumvi na majani, yafaa sana pia madini

 

Usile vichafu pia, donoa donoa hatma jutia,

Usinywe vileo pia, vyashusha afya nakwambia

Usichome chome pia, vingine utajanasia

Usifunue funue pia, vichafu visijeingia

 

Jioni pia kimbia, sikae sana tembea

Kutwaa tu kujilalia, viungo taja lemea

Puyanga pia tokwa na jasho

Kitambi unene miyeyusho.

 

Afya njema ni johari, ni vyema kujijali

Tuishi kwa tahadhari, tuombe nema za Jalali.

© Paul Mndima

Septemba 22, 2017

SHAIRI: NINA MAHABA NAWE

Standard

NINA MAHABA NAWE

nina mahaba nawe

Vile nimekaa tu chini ya mti huu,

Vile nanyewa na kunguru hapa muda huu,

Nakungoja wewe tu, kwani wakinicheka inahu?

Vile babako alinipiga rungu la mgongo,

Vile mamako alikwambia mimi muongo,

Ila bado tu nakutegea tu hapa chini ya mpingo.

Zile chabo nilikula kwenu dirishani,

Nikikuita uje kwa nje ukiwa ndani,

Akatoka baba ako na panga mkononi.

Hivi unajua ile siku navuka mto,

Kuja kwenu kukufuata mtoto,

Nilikoswa na mafuriko, waliniokoa waponda kokoto.

Ujue ile siku tuliachana totoroni,

Ile siku tulikaa mkoroshoni,

Ile mvua ilininyea yote nguoni.

Hivi wafahamu bado nadaiwa na mzee Musa,

Zile mia mbili nilizokopa nikuletee sambusa,

Na ile mia tano nilokupa alinikopa dada Shamsa.

Hivi wajua kwa nini naamka wa kwanza?

Nikiamka wa mwisho natokaje ngali nimekaza?

Wakati mwingine naamka bombo nimetoteza.

Ni vile nakuota tu yani vile nililala nakauwaza.

Vile naenda kazini mchana kutwa juani

Natembeza kahawa na ndala miguuni

Afu nakubebea vijiandazi kila jioni

Vile nakuletea maua afu mtupu tumboni

Yani vile huwa nikikuwaza nikitembea natabasamu peke yangu njiani.

Vile naandika hili shairi

Na beti napanga kwa mistari

Mishororo naipanga japo pasi urari

Taabu zote hizi sababu moja tu ukitafakari

Ni kwa sababu nina mahaba nawe Johari.

© Paul Mndima

July ‎31, ‎2017